vodacom

vodacom

Friday, February 4, 2011

Mbrazil aomba kazi Yanga

UONGOZI wa klabu ya Yanga umeanza mazungumzo na kocha kutoka nchini Brazil, Giampaulo Pedroso kwa ajili ya kuchukua nafasi ya kocha mkuu wa klabu hiyo iliyoachwa na Kostadin Papic.

Kocha huyo ambaye aliwasili hivi karibuni alishuhudia mechi kati ya Yanga na Mtibwa iliyochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga alisema wameanza mazungumzo na kocha huyo ikiwa ni mchakato wa kutafuta kocha atakayemrithi Papic.

"Tunatafuta kocha mzuri kwa ajili ya klabu yetu, zoezi la kumpata kocha mpya bado halijakamilika, kwa hiyo Pedroso yupo nchini na tutawaambia wananchi kama tutamchukua yeye au tutamuacha, ila bado tunaendelea na mzungumzo,"alisema Nchunga.

Nchunga alisema hawafanyi zoezi hilo kwa haraka na ndiyo maana wanafanya mazungumzo na makocha wengi.

"Tunatakiwa kuwa waangalifu na suala hili la kumpata kocha mpya kwa sababu kuunda benchi zuri la ufundi ni muhimu kwa timu yetu, tukimchagua kocha ambaye hana vigezo na mafunzo atatusababishia usumbufu, hatutaki kuingia kwenye usumbufu tena,"alisema Nchunga.

Naye kocha Pedroso akizungumza na Mwananchi alisema kwamba alikuwa nchini Marekani kwa miaka sita akifundisha soka kwenye academy na akiifundisha timu ya Dallas ambayo inashiriki Ligi Kuu ya Marekani inayofahamika kama Major League Soccer (MLS).

"Hivi sasa naifundisha timu inayoitwa Liverpool America na kama mapendekezo yangu ya kuomba kuifundisha Yanga yatakubaliwa nitakuja kuifundisha timu hiyo,"alisema Pedroso.

Alisema ameiona Yanga kwa dakika 90 ikicheza dhidi ya Mtibwa Sugar, ambapo amesema amegundua timu hiyo ina wachezaji wengi wenye vipaji, ila wanakosa mambo ya kiufundi hasa hasa katika ushambuliaji.

"Yanga walitawala mechi ile, walitengeneza nafasi nyingi, ila kufunga ilikuwa ni tatizo, wanatakiwa kuwa makini katika ufungaji na kufanya mabadiliko madogo, nina matumaini Yanga itakuwa timu nzuri kabisa,"alisema Pedroso

No comments:

Post a Comment