vodacom

vodacom

Wednesday, February 9, 2011

Poulsen: Tupo tayari kucheza na Palestina

Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Jan B Poulsem amesema timu yake ipo tayari kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya Taifa ya Palestina unaotarajiwa kufanyika kesho katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Amesema mchezo huo wa kirafiki unaoandaliwa na Shirkisho la Mpira wa Miguu duniani FIFA utatumika kama sehemu ya matayarisho kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa hatua ya pili wa fainali za kombe la mataifa ya Afrika dhidi ya timu ya Afrika ya Kati utakaochezwa mwezi ujao.

“Tumejiandaa kucheza mchezo huo, wachezaji wa Yanga wataingia kambini leo mchana, lakini hata wasipoingia lazima tucheze mchezo huo, tupo katika maandalizi hivyo mechi yoyote ni muhimu kwetu.” alisema Poulsen.

Ameongeza kuwa akiwa hafahamu utaratibu unaotumika na FIFA wa kutoa viwango vya timu duniani, atacheza mchezo huo kwa kuwa tayari timu ya Palestina kutoka nchi za Kiarabu imewasili kwa ajili ya mchezo huo.
Akiizungumzia mechi hiyo Poulsen amesema Palestina ni timu nzuri na yenye kucheza mchezo mzuri hivyo kuwa nyuma katika viwango vya FIFA haitaifanya Stars kuidharau mechi hiyo.

Naye kocha wa Palestina Bezaz Moussa amesema wanashukuru kupata nafasi ya kucheza na Tanzania , nchi ambayo ipo katika mchakato wa kukuza soka lake, hivyo mchezo wa kesho utakuwa mgumu kwao.

“Tumeifahamu zaidi Tanzania kupitia katika mchezo wake dhidi ya Algeria , ni timu nzuri na bora kwetu, tutajitahidi kupata ushindi na kucheza mchezo mzuri kwani timu yangu inawachezaji mahiri na wazuri.”alisema Moussa.

Kocha Moussa ameongeza kuwa timu yake inapata uzoefu zaidi wa mechi za kimataifa, imeshacheza mechi nyingi zikiwemo Botania na Sudan ambazo walitoka sare ya 1-1 huku wakifungwa 3-0 na Iraq.

Mchezo wa kesho unatarajiwa kuchezwa jioni majira ya saa 11, kukiwa na viingilio kuanzania kiwango cha shilingi 1,000 hadi 10,000.

No comments:

Post a Comment