vodacom

vodacom

Thursday, February 3, 2011

Amboni pana mapango 70

KUNA simulizi nyingi kuhusu Mapango ya Amboni ambayo kwa mujibu wa Mhifadhi Mambo ya Kale Amboni, Jumanne Maburi yalitokana na athari ya miamba hiyo kufurika maji yapata miaka 150milioni iliyopita.

Ipo ile ya miaka ya 1940, inayosema kwamba kulikuwa na wazungu wawili, mke na mume walioingia na mbwa kinyume na masharti ili awalinde. Hawakurudi, walipotelea humo. Inadaiwa kwamba mbwa wao alipita chini kwa chini na kutokea Kilimanjaro!

Simulizi nyingine ni ile inayosema kwamba kuna njia katika mapango hayo inayotokea Mombasa. Hata hivyo, Maburi anasema simulizi zote hizo hazijathibitishwa kitaalamu... "Wataalamu waliwahi kufuatilia na baada ya mita tano hapakuwa na njia inayoendelea. Hadi sasa hatuwezi kusema kwamba simulizi hizo zina ukweli."

Lakini kuna mambo ya kusisimua katika mapango hayo, licha ya watalii wa ndani na nje kuyatembelea, wengine zaidi ya mara mbili, kila wakati wakifika hupata jipya na hata yale waliyoyaona yanakuwa kama mageni machoni mwao.

Miamba hiyo ina mambo! Kuna maeneo ambayo yamechongeka katika maumbo mbalimbali ambayo yanafanana au kufananishwa na maeneo ya kijiografia au maumbile ya mwanadamu, wanyama na masuala ya kiimani.

Kwa mfano, kuna eneo ambalo linafananishwa na Kibla, Sanamu ya Bikira Maria, Sanamu ya Mnara wa Uhuru (Liberty) wa Washington, Marekani.

Maeneo hayo unaanza kuyaona hata kabla ya kutia mguu kuingia pangoni. Mhifadhi Maburi baada ya kutoa maelezo ya utangulizi na kisha kuchukua zana ya kuingia nayo pangoni (tochi kubwa) alichukua fimbo kubwa iliyokuwa katika eneo lililotengwa maalumu kwa ajili ya kuanza ziara ya kutembelea eneo hilo.

"Mnaona hapa (akionyesha eneo la wazi juu ya lango hilo. Mnadhani panafanana na kitu gani?" Jibu halikuwa gumu kwani karibu watalii wote tuliokuwamo katika msafara ule tulibaini bila ya shaka kwamba ile ilikuwa kama ramani ya Bara la Afrika.

Akauliza tena, akigeukia upande wake wa kulia... "Na hapa mnaona kitu gani?" Pale kulikuwa na mwamba mkubwa ambao kwa mbele umechongwachongwa. Hapakuwa na jibu la moja kwa moja, wapo waliosema ni nyati, mbogo lakini hata kabla mhifadhi huyo hajatoa jibu, kundi kubwa likasema simba. Akasema naam, safari ya kuingia ndani ikaanza.

Licha ya kwamba kulikuwa na giza nene na kona nyingi, sehemu ile ya mwanzo ilikuwa na hali ya ubaridi, hali hiyo ilikuwa ikibadilikabadilika kadri tulivyokuwa tukifika katika eneo moja hadi jingine. Kuna maeneo mengine ambayo baadhi walitamani kurudi lakini hakuna aliyethubutu kufanya hivyo, kona zote zile na giza wangeanzia wapi!

Kuna sehemu tulilazimika kutambaa na kama ulikuwa wa mwisho na simu yako haina tochi ilikuwa burudani ya aina yake. Humo ndani kuna eneo linaloitwa Kilimanjaro, unapanda hadi kileleni lakini bila ya kutoka nje, ni kama ghorofani na kuna sehemu ambayo watalii hufanya sherehe mbalimbali wakiwa ndani, hapo kuna mwanga kwa mbali unaotokea katika tundu moja lililoko juu, hewa yake ni nzuri mithili ya kiyoyozi. Hakika panastahili.

Pembeni mwa eneo hilo kulikuwa na eneo ambalo mchongo wake unafanana na Kibla (Al-Kaaba) ya msikiti. Pembeni yake, alituonyesha michoro ambayo inafanana kama maandishi ya Kiarabu

Tulifika eneo jingine ambalo alimulika tochi yake kwa juu akatuonyesha alama nyingine... "Mnaona kule juu? Ile ni sanamu Sanamu ya Bikra Maria!" Watalii wengi walionekana kukubaliana naye moja kwa moja.

Lipo eneo tuliloona vitu kama ubani na udi ambalo tuluelezwa na mhifadhi kwamba ni eneo la kutambikia. Awali, alitueleza kwamba pango hilo tuliloingia linajulikana pia kama Pango la Mzimu wa Mabavu.

Sehemu nyingine tuliona nyayo za binadamu lakini zikiwa darini, kulikuwa pia na michongo mingine kama ya sanamu ya meli na miamba mingine inayoota baadhi ikiwa meupa na inayong'ara.

Ziara yetu katika pango hilo la mizimu ya mabavu ilihitimishwa kwa kupanda ndege. Mfifadhi yule alitutaka tuingie katika 'ndege' tayari kwa kuanza safari ya kwenda kusikojulikana. Lilikuwa ni eneo la kupanda ngazi sehemu yake ya kuingilia ilikuwa mithili ya milango ya ndege..." Mkisha ingia humu, kama rubani amelala msimwamshe..." alitania mhifadhi.

Hamad, baada ya kuingia ndani ya 'ndege' hiyo, tulijikuta tukiwa nje ya pango karibu kabisa na pale tulipoingilia. Wakati tukishangaa, mhifadhi Maburi alitokea kwa upande mwingine! Sote tukaangua kicheko cha furaha. Ilikuwa ziara ya nusu saa iliyojaa kila aina ya msisimko.

Lakini Maburi alitueleza jambo ambalo lilitushtua watalii tuliokuwapo pale, anasema eneo hilo la Mapango ya Amboni ambalo ukubwa wake ni zaidi ya hekta za mraba 250, halitumiki inavyostahili.

"Kuna pango jingine linalotumika. Linaitwa Pango la Jjinsia. humo kuna michoro ya maumbile yanayofanana na ya via za uzazi za binadamu yaani uume na uke."

Lakini Maburi anasema Amboni pana mapango zaidi ya 70 ingawa yanayotumika kwa shughuli za kitalii ni hayo mawili tu. Tulidhani pengine tatizo ni usalama pekee lakini anasema la hasha...

"Hapa tupo wahifadhi watatu tu. Hakuna waongozaji wa watalii kazi hiyo pia tunaifanya sisi. Mjini kuna kampuni za utalii lakini hawazitumii."

No comments:

Post a Comment