MWENYEKITI wa klabu ya Yanga, Llyod Nchunga amesema aliyekuwa kocha wa timu hiyo Kostadin Papic ametoroka nchini bila kukabidhi baadhi ya ripoti ya taarifa za wachezaji.
Vyombo vya habari mbalimbali jana viliripoti kuwa uongozi wa Yanga ulimpa masharti matatu Papic na kwamba ulitaka atoe ufafanuzi wa baadhi ya mambo ndio aondoke.
Lakini badala yake saa nne usiku wa kuamkia jana, kocha huyo aliripotiwa kuondoka na Nchunga jana aliwaambia waandishi wa habari kuwa Papic alitoroka kwani yeye kama Mwenyekiti hakuwa na taarifa za kuondoka kwake licha ya kuwepo kwa madai kuwa kocha huyo alimuaga Makamu wake Davis Mosha.
Baadhi ya masharti ambayo uongozi wa Yanga ulimtaka Papic kutoa ufafanuzi kwa mfadhili wao Yusuf Manji ni kwanini aliitia hasara klabu kwa kumsajili mchezaji Keneth Asamoah na badala yake asiweze kuichezea timu hiyo, mchakato wa fedha za usajili wa wachezaji na pia kutoa maelezo ya fedha za usajili za kipa Ivan Knezevic Sh milioni 3.7.
Inadaiwa kuwa Papic alikopa Sh milioni nne kwa uongozi wa Yanga na ilipofika wakati wa kuzirudisha alisema kwamba atampa Knezevic lakini mpaka siku mbili kabla ya kocha huyo kutoroka kipa huyo alikuwa hajapewa fedha zake.
“Kuna ufisadi zaidi uliofanyika kwenye sakata la usajili kwa kuwa kuna baadhi ya wachezaji walioripotiwa kuwa wamepewa fedha za usajili Sh milioni 15 lakini wachezaji hao wamepewa sh milioni kumi,” alisema.
Alisema kuwa kwa sasa uongozi wa klabu hiyo unaendelea na hatua zake za kawaida za kufuatilia ukaguzi wa hesabu za klabu.
Akizungumzia hatua ambayo klabu inachukua kutafuta kocha, Nchunga alisema kuwa uongozi wake ulikuwa na mazungumzo na Sam Timbe ili kuangalia kama anaweza kupewa mikoba ya Papic.
Pia aliongeza kuwa makocha kutoka nchi mbalimbali walioomba kuinoa Yanga na tayari wametuma CV zao kwenye mtandao.
Makocha hao ni Roy Barreto wa Uingereza, Simeon Afremov wa Yugoslavia na Ivo Von wa Slovenia.
Wakati huohuo, Nchunga jana alimtangaza Mwesigwa Selestine kuwa Kaimu Katibu Mkuu wa klabu hiyo baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Katibu Mkuu Lawrance Mwalusako.
Alisema uteuzi wa Mwesigwa ulifanyika juzi na kwamba Kaimu Katibu huyo ni mwanachama wa Yanga mwenye kadi namba 004010 na ana uhusiano na mitandao mingi duniani ijishugulishayo na mchezo wa soka ikiwa pamoja na kuendeleza soka la vijana.

No comments:
Post a Comment